Jua lilipozama, anga likachorwa kwa rangi za moto na uturi, giza likashuka kama pazia zito na kufunika nchi nzima. Mgao wa umeme uliacha mitaa ya uswahilini ikihema kwa mwanga hafifu wa mbalamwezi kama macho ya paka mwenye kukaribia umauti.
Bwana Hoi bin Taaban alikatiza mitaa ya uswahilini akisindikizwa na msongo wa mawazo. Alitembea kama ndege aliyepoteza mabawa huku nyayo zake zikilalama maumivu ya kutembea peku lakini moyo wake ukiifurahia kila hatua aliyoipiga, kwani kila hatua ilimfanya akaribie kuliona tabasamu la mkewe.
Tabasamu ambalo kwake lilikuwa kama jua la alfajiri, linalofukuza giza la huzuni moyoni. Kama upepo wa pwani, unaotuliza mawimbi ya mawazo akilini. Kama nyota iliyosalia angani baada ya wingu zito la mawazo kutanda. Kama chemchemi ya matumaini katika jangwa la moyo uliopigwa na kiangazi cha shida. Kama ua la waridi linalochanua katikati ya miiba.
Bwana Hoi hakuwa na uwezo wa kumnunulia mke wake mavazi ya kifahari kama ya majirani. Waliovaa silki za Italia na abaya za Uarabuni, na kunukia kwa manukato ya ughaibuni. Wala nyayo zao hazikugusa michanga au nyuso zao kutaabishwa juani. Ilikuwa si ajabu kwa wawili hao kulala njaa na kuamka na kiu, lakini tabasamu la mke wake halikuwahi kuwa mbali.
Bwana Hoi alijua kuwa furaha ya mkewe ilikuwa kama hazina, yenye thamani kuliko chochote. Kuilinda hazina hiyo, akatafakari nini afanye kujikwamua kiuchumi.
Sauti za mbwa zikalalama kwa ukali na kumtoa mawazoni. Bwana Hoi akashika mfuko wake kwa nguvu, mfuko uliokuwa na gauni zuri lililokunjwa kwa ustadi kama zawadi ya harusi. Mzigo huo haukupimwa kwa uzito wa kilo, bali kwa thamani ya upendo. Ulinunuliwa kwa jasho la kazi ngumu, posho ya muhindi iliyopatikana kwa mateso na masimango.
Ghafla, kelele zikalipuka. Duka jirani lilikuwa limevunjwa. Mayowe ya umati yakasonga kama mawimbi ya hasira. Kundi lile la watu wengi lilipomuona Bwana Hoi, maskini mwenye mavazi duni, ameshikilia mfuko wa zawadi, wakamtambua lakini swali hakuulizwa, wala maelezo yake kungojewa.
Majirani wakamvamia. Wakamwangusha kama mzigo, wakampiga na kumtukana. “Mchomeeni! Mwizi hapaswi kuhurumiwa!” Macho yake yakiwa na mshangao wa hofu, akaushika mfuko wake kama pumzi yake ya mwisho. Akakimbia, si kwa hatia bali kwa hofu ya kufa kabla ya kumpa mke wake zawadi.
Akihema kama roho inamtoka, akaikaribia nyumba yake. Alijua mke wake alikuwa akimngojea Lakini, hatua chache kabla ya kufika, walimkamata tena. Rungu zito lilipiga shingo yake, likizima taa ya fahamu. Matairi yakaletwa, mafuta yakamwagwa, kibiriti kikashikwa. Lakini bado, alishikilia mfuko wake. Kwa mbali sauti ya mwanamke mwenye asili ya kichaga ikasikika ikifoka na kurudia maneno. “Huyo si mwizi! Mwacheni! Bwana Hoi sio mwizi!”
Alikuwa mmiliki wa duka lililovunjwa, jirani aliyemfahamu Bwana Hoi bin Taaban. Ajabu Sauti ya Mwanamke huyo haikuwa kubwa kuzidi hasira za watu waliochoshwa na matukio mengi ya wizi katika mitaa ya uswahilini . Kibiriti kikadondoka mikononi mwa kaduguda na moto ukasafiri kwa kasi kama upepo na kushika mwili wa Bwana Hoi Bin Taaban.
Kilio cha mke wake kilipasua anga la usiku, kama tarumbeta ya mwisho isikikayo siku ya hukumu. Alianguka pembeni mwa mwili wa mumewe, moto ukichoma ngozi yake kwa mapenzi yasiyopimika. Alimkumbatia Bwana Hoi kwa taulo zito lenye maji mengi, akalia kwa nguvu kama vile alitaka machozi yake yazime moto kwa haraka.
Kwa michanga na maji, kundi lile likajaribu kuwaokoa wapenzi hao, na japokuwa walifanikiwa kuuzima, moto ulikuwa tayari umefanya kazi yake. Walimwangalia yule mama, ambaye sasa alikuwa ameketi ardhini, akimlisha machozi mumewe aliyekuwa amedhoofu huku mikono yake ikiwa imeshikilia gauni lililoungua. Kwa mke wake, zawadi ile ilikuwa na thamani sawa na uhai wa mume wake.
Bwana Hoi akamuangalia mkewe na kulitafuta tabasamu usoni mwake. Hata lile lililochorwa kwa machungu na kufichwa kwa kinyago cha faraja, hakuliona. Huzuni ilitanda kama ukungu mzito machoni mwa mke wake, uso wa mkewe ulijawa na hofu isiyoelezeka. Bwana Hoi akasema kwa sauti dhaifu: “Samahani, sikuweza kukupa maisha mazuri, lakini nilitamani sana.”
Mkewe alimtazama kwa macho yaliyojaa mapenzi yasiyoisha, akajibu: “Upendo wako ulinitosha, hakuna siku niliyopungukiwa furaha.”
Bwana Hoi, akijua asingeweza kuiona kesho wala kutimiza ndoto zake, akasema,”Naomba utabasamu, mke wangu.”
Mvua ikashuka, kana kwamba anga liliomboleza kifo cha shujaa na kuficha machozi kwenye paji la uso wa mke wake. Watu wakaanza kuondoka mmoja baada ya mwingine, aibu ikiwa imewafunga midomo. Hakuna aliyethubutu kumtazama yule mama, aliyekuwa ameketi ardhini, akimkumbatia mumewe aliyekuwa amedhoofu.
Japokuwa alijaribu kutabasamu, alishindwa. Bwana Hoi bin Taaban, maskini wa mali na tajiri wa moyo, aliaga dunia, na tabasamu la mke wake lilikuwa limezimika milele. Kilio cha mke wake kilipasua anga la usiku, kikifunikwa kwa sauti kubwa za milio ya radi. Alimkumbatia mumewe kwa nguvu, akilia kwa uchungu usiopimika. Machozi yake yalichanganyika na mvua, yakimwagika kama mito ya huzuni. Kwake, maisha yalipoteza maana
7 Responses
The story is so 👌👌 but a sad ending…..I need continuation
Thank you
Waow …amazing
Asante sana
Awesome https://lc.cx/xjXBQT
Very good https://is.gd/N1ikS2
Very good https://is.gd/N1ikS2